13
Hasira Ya Bwana Dhidi Ya Israeli 
 1 Wakati Efraimu alipozungumza, watu walitetemeka, 
alikuwa ametukuzwa katika Israeli. 
Lakini alikuwa na hatia ya kumwabudu Baali 
naye akafa. 
 2 Sasa wanatenda dhambi zaidi na zaidi; 
wanajitengenezea sanamu 
kutokana na fedha yao, 
vinyago vilivyotengenezwa kwa uhodari, 
vyote kazi ya fundi stadi. 
Inasemekana kuhusu hawa watu, 
“Hutoa dhabihu za binadamu 
na kubusu sanamu za ndama.” 
 3 Kwa hiyo watakuwa kama ukungu wa asubuhi, 
kama umande wa alfajiri utowekao, 
kama makapi yapeperushwayo 
kutoka sakafu ya kupuria nafaka, 
kama moshi utorokao kupitia dirishani. 
 4 “Bali mimi ndimi Bwana Mungu wenu, 
niliyewaleta ninyi toka Misri. 
Msimkubali Mungu mwingine ila mimi, 
hakuna Mwokozi isipokuwa mimi. 
 5 Niliwatunza huko jangwani, 
katika nchi yenye joto liunguzalo. 
 6 Nilipowalisha, walishiba, 
waliposhiba, wakajivuna, 
kisha wakanisahau mimi. 
 7 Kwa hiyo nitakuja juu yao kama simba, 
kama chui nitawavizia kando ya njia. 
 8 Kama dubu aliyenyangʼanywa watoto wake, 
nitawashambulia na kurarua vifua vyenu. 
Kama simba nitawala; 
mnyama pori atawararua vipande vipande. 
 9 “Ee Israeli, umeangamizwa, 
kwa sababu wewe u kinyume nami, 
kinyume na msaidizi wako. 
 10 Yuko wapi mfalme wako, 
ili apate kukuokoa? 
Wako wapi watawala wako katika miji yako yote 
ambao ulisema kuwahusu, 
‘Nipe mfalme na wakuu’? 
 11 Hivyo katika hasira yangu nilikupa mfalme 
na katika ghadhabu yangu nilimwondoa. 
 12 Kosa la Efraimu limehifadhiwa, 
dhambi zake zimewekwa katika kumbukumbu. 
 13 Utungu kama wa mwanamke anayejifungua mtoto humjia, 
lakini yeye ni mtoto asiyekuwa na hekima; 
wakati utakapowadia hatatoka 
katika tumbo la mama yake. 
 14 “Nitawakomboa watu hawa kutoka nguvu za kaburi, 
nitawakomboa kutoka mautini. 
Yako wapi, ee mauti, mateso yako? 
Uko wapi, ee kuzimu, uharibifu wako? 
“Sitakuwa na huruma, 
 15 hata ingawa Efraimu atastawi 
miongoni mwa ndugu zake. 
Upepo wa mashariki kutoka kwa Bwana utakuja, 
ukivuma kutoka jangwani, 
chemchemi yake haitatoa maji 
na kisima chake kitakauka. 
Ghala lake litatekwa 
hazina zake zote. 
 16 Watu wa Samaria ni lazima wabebe hatia yao, 
kwa sababu wameasi dhidi ya Mungu wao. 
Wataanguka kwa upanga; 
watoto wao wadogo watatupwa kwa nguvu ardhini, 
wanawake wao walio na mimba watatumbuliwa.”