11
Upendo Wa Mungu Kwa Israeli 
 1 “Wakati Israeli alipokuwa mtoto, nilimpenda, 
nilimwita mwanangu kutoka Misri. 
 2 Lakini kadiri nilivyomwita Israeli, 
ndivyo walivyokwenda mbali nami. 
Walitoa dhabihu kwa Mabaali 
na kufukiza uvumba kwa vinyago. 
 3 Mimi ndiye niliyemfundisha Efraimu kutembea, 
nikiwashika mikono; 
lakini hawakutambua 
kuwa ni mimi niliyewaponya. 
 4 Niliwaongoza kwa kamba za huruma ya kibinadamu, 
kwa vifungo vya upendo; 
niliondoa nira shingoni mwao 
nami nikainama kuwalisha. 
 5 “Je, hawatarudi Misri, 
nayo Ashuru haitawatawala 
kwa sababu wamekataa kutubu? 
 6 Panga zitametameta katika miji yao, 
zitaharibu makomeo ya malango yao 
na kukomesha mipango yao. 
 7 Watu wangu wamedhamiria kuniacha. 
Hata kama wakimwita Yeye Aliye Juu Sana, 
kwa vyovyote hatawainua. 
 8 “Efraimu, ninawezaje kukuacha? 
Ee Israeli, ninawezaje kukutoa? 
Nitawezaje kukutendea kama Adma? 
Nitawezaje kukufanya kama Seboimu? 
Moyo wangu umegeuka ndani yangu, 
huruma zangu zote zimeamshwa. 
 9 Sitatimiza hasira yangu kali, 
wala sitageuka na kumharibu Efraimu. 
Kwa kuwa mimi ndimi Mungu, 
wala si mwanadamu, 
Aliye Mtakatifu miongoni mwenu. 
Sitakuja kwa ghadhabu. 
 10 Watamfuata Bwana; 
atanguruma kama simba. 
Wakati angurumapo, 
watoto wake watakuja wakitetemeka 
kutoka magharibi. 
 11 Watakuja wakitetemeka 
kama ndege wakitoka Misri, 
kama hua wakitoka Ashuru. 
Nitawakalisha katika nyumba zao,” 
asema Bwana. 
Dhambi Ya Israeli 
 12 Efraimu amenizunguka kwa uongo, 
nyumba ya Israeli kwa udanganyifu. 
Naye Yuda ni mkaidi dhidi ya Mungu, 
hata kinyume cha yule mwaminifu Aliye Mtakatifu.