2
Mpendwa 
 1 Mimi ni ua la Sharoni, 
yungiyungi ya bondeni. 
Mpenzi 
 2 Kama yungiyungi katikati ya miiba 
ndivyo alivyo mpenzi wangu katikati ya wanawali. 
Mpendwa 
 3 Kama mti wa mtofaa miongoni mwa miti ya msituni 
ndivyo alivyo mpenzi wangu 
miongoni mwa wanaume vijana. 
Ninafurahia kuketi kivulini mwa mwanaume huyu, 
na tunda lake ni tamu kwangu. 
 4 Amenichukua mpaka kwenye ukumbi wa karamu, 
na bendera ya huyu mwanaume 
juu yangu ni upendo. 
 5 Nitie nguvu kwa zabibu kavu, 
niburudishe kwa matofaa, 
kwa maana ninazimia kwa mapenzi. 
 6 Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, 
na mkono wake wa kuume unanikumbatia. 
 7 Binti za Yerusalemu, ninawaagiza 
kwa paa na kwa ayala wa shambani: 
Msichochee wala kuamsha mapenzi 
hata yatakapotaka yenyewe. 
Shairi La Pili 
Mpendwa 
 8 Sikiliza! Mpenzi wangu! 
Tazama! Huyu hapa anakuja, 
akirukaruka juu milimani 
akizunguka juu ya vilima. 
 9 Mpenzi wangu ni kama paa au ayala kijana. 
Tazama! Anasimama nyuma ya ukuta wetu, 
akitazama kupitia madirishani, 
akichungulia kimiani. 
 10 Mpenzi wangu alizungumza na kuniambia, 
“Inuka, mpenzi wangu, 
mrembo wangu, tufuatane. 
 11 Tazama! Wakati wa masika umepita, 
mvua imekwisha na ikapita. 
 12 Maua yanatokea juu ya nchi; 
majira ya kuimba yamewadia, 
sauti za njiwa zinasikika 
katika nchi yetu. 
 13 Mtini unatunga matunda yake ya mwanzoni, 
zabibu zinazochanua zaeneza harufu nzuri. 
Inuka, njoo mpenzi wangu. 
Mrembo wangu, tufuatane.” 
Mpenzi 
 14 Hua wangu penye nyufa za majabali, 
mafichoni pembezoni mwa mlima, 
nionyeshe uso wako, 
na niisikie sauti yako, 
kwa maana sauti yako ni tamu, 
na uso wako unapendeza. 
 15 Tukamatie mbweha, 
mbweha wale wadogo 
wanaoharibu mashamba ya mizabibu, 
mashamba yetu ya mizabibu yaliyochanua. 
Mpendwa 
 16 Mpenzi wangu ni wangu, nami ni wake, 
yeye hujilisha katikati ya yungiyungi. 
 17 Mpaka jua linapochomoza, 
na vivuli vikimbie, 
rudi, mpenzi wangu, 
na uwe kama paa, 
au kama ayala kijana 
juu ya vilima vya Betheri.