4
Elifazi Anazungumza: Ayubu Ametenda Dhambi 
 1 Ndipo Elifazi Mtemani akajibu: 
 2 “Kama mtu akithubutu kuzungumza nawe, 
kutakukasirisha? 
Lakini ni nani awezaye 
kujizuia asiseme? 
 3 Fikiri jinsi ambavyo umewafundisha watu wengi, 
jinsi ambavyo umeitia nguvu 
mikono iliyokuwa dhaifu. 
 4 Maneno yako yamewategemeza wale waliojikwaa; 
umeyatia nguvu magoti yaliyokuwa dhaifu. 
 5 Lakini sasa hii taabu imekujia wewe, 
nawe unashuka moyo; 
imekupiga wewe, 
nawe unafadhaika. 
 6 Je, kumcha Mungu kwako hakupaswi kuwa 
ndiyo matumaini yako 
na njia zako kutokuwa na lawama 
ndilo taraja lako? 
 7 “Fikiri sasa: Ni mtu yupi asiye na hatia ambaye aliwahi kuangamia? 
Ni wapi wanyofu waliwahi kuangamizwa? 
 8 Kwa jinsi ambavyo mimi nimechunguza, 
wale walimao ubaya 
na wale hupanda uovu, 
huvuna hayo hayo hayo. 
 9 Kwa pumzi ya Mungu huangamizwa; 
kwa mshindo wa hasira zake huangamia. 
 10 Simba anaweza kunguruma na kukoroma, 
lakini bado meno ya simba mkubwa huvunjika. 
 11 Simba anaweza kuangamia kwa kukosa mawindo, 
nao wana wa simba jike hutawanyika. 
 12 “Neno lililetwa kwangu kwa siri, 
masikio yangu yakasikia mnongʼono wake. 
 13 Katikati ya ndoto za kutia wasiwasi wakati wa usiku, 
hapo usingizi mzito uwapatapo wanadamu, 
 14 hofu na kutetemeka kulinishika 
na kufanya mifupa yangu yote itetemeke. 
 15 Kuna roho aliyepita mbele ya uso wangu, 
nazo nywele za mwili wangu zikasimama. 
 16 Yule roho akasimama, 
lakini sikuweza kutambua kilikuwa kitu gani. 
Umbo fulani lilisimama mbele ya macho yangu, 
kukawa na ukimya kisha nikasikia sauti: 
 17 ‘Je, binadamu aweza kuwa mwadilifu kuliko Mungu? 
Je, mtu aweza kuwa safi kuliko Muumba wake? 
 18 Kama Mungu hawaamini watumishi wake, 
kama yeye huwalaumu malaika zake kwa kukosea, 
 19 ni mara ngapi zaidi wale waishio katika nyumba 
za udongo wa mfinyanzi, 
ambazo misingi yake ipo mavumbini, 
ambao wamepondwa kama nondo! 
 20 Kati ya mawio na machweo 
huvunjwa vipande vipande; 
bila yeyote kutambua, 
huangamia milele. 
 21 Je, kamba za hema yao hazikungʼolewa, 
hivyo hufa bila hekima?’