2
Faida Za Hekima 
 1 Mwanangu, kama utayakubali maneno yangu 
na kuyaweka akiba maagizo yangu ndani mwako, 
 2 kutega sikio lako kwenye hekima 
na kuweka moyo wako katika ufahamu, 
 3 na kama ukiita busara 
na kuita kwa sauti ufahamu, 
 4 na kama utaitafuta kama fedha 
na kuitafuta sana kama hazina iliyofichwa, 
 5 ndipo utakapoelewa kumcha Bwana 
na kupata maarifa ya Mungu. 
 6 Kwa maana Bwana hutoa hekima, 
na kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu. 
 7 Anahifadhi ushindi kwa ajili ya mwadilifu, 
yeye ni ngao kwa wale wasio na lawama, 
 8 kwa kuwa hulinda mwenendo wa mwenye haki 
na kuhifadhi njia ya waaminifu wake. 
 9 Ndipo utafahamu lipi lililo kweli na haki 
na sawa: yaani kila njia nzuri. 
 10 Kwa maana hekima itaingia moyoni mwako, 
nayo maarifa yataifurahisha nafsi yako. 
 11 Busara itakuhifadhi 
na ufahamu utakulinda. 
 12 Hekima itakuokoa kutoka njia za waovu, 
kutoka kwa watu ambao maneno yao yamepotoka, 
 13 wale waachao mapito yaliyonyooka 
wakatembea katika njia za giza, 
 14 wale wapendao kutenda mabaya 
na kufurahia upotovu wa ubaya, 
 15 ambao mapito yao yamepotoka 
na ambao ni wapotovu katika njia zao. 
 16 Itakuokoa pia kutokana na mwanamke kahaba, 
kutokana na mke aliyepotoka mwenye maneno 
ya kushawishi kutenda ubaya, 
 17 aliyemwacha mwenzi wa ujana wake 
na kupuuza agano alilofanya mbele ya Mungu. 
 18 Kwa maana nyumba yake huelekea kwenye kifo 
na mapito yake kwenye roho za waliokufa. 
 19 Hakuna yeyote aendaye kwake akarudi, 
au kufikia mapito ya uzima. 
 20 Hivyo utatembea katika njia za watu wema 
na kushikamana na mapito ya wenye haki. 
 21 Kwa maana wanyofu wataishi katika nchi, 
nao wasio na lawama watabakia ndani yake. 
 22 Bali waovu watakatiliwa mbali kutoka nchi, 
nao wasio waaminifu watangʼolewa kutoka humo.