Zaburi 146
Kumsifu Mungu Mwokozi 
Ee nafsi yangu, umsifu Bwana, 
 2 Nitamsifu Bwana maisha yangu yote; 
nitamwimbia Mungu wangu sifa 
wakati wote niishipo. 
 3 Usiweke tumaini lako kwa wakuu, 
kwa wanadamu ambao hufa, 
ambao hawawezi kuokoa. 
 4 Roho yao itokapo hurudi mavumbini, 
siku hiyo hiyo mipango yao yote hukoma. 
 5 Heri yeye ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake, 
ambaye tumaini lake ni katika Bwana, Mungu wake, 
 6 Muumba wa mbingu na nchi, 
na bahari na vyote vilivyomo ndani yake: 
Bwana anayedumu kuwa mwaminifu 
milele na milele. 
 7 Naye huwapatia haki walioonewa 
na kuwapa wenye njaa chakula. 
Bwana huwaweka wafungwa huru, 
 8  Bwana huwafumbua vipofu macho, 
Bwana huwainua waliolemewa na mizigo yao, 
Bwana huwapenda wenye haki. 
 9  Bwana huwalinda wageni 
na kuwategemeza yatima na wajane, 
lakini hupinga njia za waovu. 
 10  Bwana atamiliki milele, 
Mungu wako, ee Sayuni, 
kwa vizazi vyote. 
Msifuni Bwana.