15
Unabii Dhidi Ya Moabu 
 1 Neno kuhusu Moabu: 
Ari iliyo Moabu imeangamizwa: 
imeharibiwa kwa usiku mmoja! 
Kiri iliyo Moabu imeangamizwa, 
imeharibiwa kwa usiku mmoja! 
 2 Diboni anakwea hadi kwenye hekalu lake, 
mpaka mahali pake pa juu ili walie, 
Moabu anaombolezea Nebo na Medeba. 
Kila kichwa kimenyolewa 
na kila ndevu limeondolewa. 
 3 Wamevaa nguo za magunia barabarani, 
juu ya mapaa na kwenye viwanja 
wote wanaomboleza, 
wamelala kifudifudi kwa kulia. 
 4 Heshboni na Eleale wanalia, 
sauti zao zinasikika hadi Yahazi. 
Kwa hiyo watu wenye silaha wa Moabu wanapiga kelele, 
nayo mioyo yao imezimia. 
 5 Moyo wangu unamlilia Moabu; 
wakimbizi wake wanakimbilia Soari, 
hadi Eglath-Shelishiya. 
Wanapanda njia ya kwenda Luhithi, 
wanakwenda huku wanalia; 
barabarani iendayo Horonaimu 
wanaombolezea maangamizi yao. 
 6 Maji ya Nimrimu yamekauka 
na majani yamenyauka; 
mimea imekauka wala hakuna 
kitu chochote kibichi kilichobaki. 
 7 Kwa hiyo mali waliyoipata na kujiwekea akiba 
wamezichukua na kuvuka Bonde la Mierebi. 
 8 Mwangwi wa kilio chao umefika hadi mpakani mwa Moabu, 
kilio chao cha huzuni kimefika hadi Eglaimu, 
maombolezo yao hadi Beer-Elimu. 
 9 Maji ya Dimoni yamejaa damu, 
lakini bado nitaleta pigo jingine juu ya Dimoni: 
simba juu ya wakimbizi wa Moabu 
na juu ya wale wanaobaki katika nchi.