Swahili New Testament Bible

Luke 7

Luke

Return to Index

Chapter 8

1

Baada ya hayo, Yesu alipitia katika miji na vijiji akitangaza Habari Njema za Ufalme wa Mungu. Wale kumi na wawili waliandamana naye.

2

Pia wanawake kadhaa ambao Yesu alikuwa amewatoa pepo wabaya na kuwaponya magonjwa, waliandamana naye. Hao ndio akina Maria (aitwaye Magdalene), ambaye alitolewa pepo wabaya saba;

3

Yoana, mke wa Kuza, mfanyakazi mkuu wa Herode; Susana na wengine kadhaa. Hao wanawake walikuwa wakiwatumikia kwa mali yao wenyewe.

4

Kundi kubwa la watu lilikuwa linakusanyika, na watu walikuwa wanamjia Yesu kutoka kila mji. Naye akawaambia mfano huu:

5

"Mpanzi alikwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akipanda zile mbegu, nyingine zilianguka njiani, na wapita njia wakazikanyaga, na ndege wakazila.

6

Nyingine zilianguka penye mawe, na baada ya kuota zikanyauka kwa kukosa maji.

7

Nyingine zilianguka kati ya miti ya miiba. Ile miti ya miiba ilipoota ikazisonga.

8

Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikaota na kuzaa asilimia mia." Baada ya kusema hayo, akapaaza sauti, akasema, "Mwenye masikio na asikie!"

9

Wanafunzi wake wakamwuliza Yesu maana ya mfano huo.

10

Naye akajibu, "Ninyi mmejaliwa kujua siri za Ufalme wa Mungu, lakini hao wengine sivyo; ila hao huambiwa kwa mifano, ili wakitazama wasiweze kuona, na wakisikia wasifahamu.

11

"Basi, maana ya mfano huu ni hii: mbegu ni neno la Mungu.

12

Zile zilizoanguka njiani zinaonyesha watu wale wanaosikia lile neno, halafu Ibilisi akaja na kuliondoa mioyoni mwao wasije wakaamini na hivyo wakaokoka.

13

Zile zilizoanguka penye mawe zinaonyesha watu wale ambao wanaposikia juu ya lile neno hulipokea kwa furaha. Hata hivyo, kama zile mbegu, watu hao hawana mizizi maana husadiki kwa kitambo tu, na wanapojaribiwa hukata tamaa.

14

Zile zilizoanguka kwenye miti ya miiba ni watu wale wanaosikia lile neno, lakini muda si muda, wanapokwenda zao, husongwa na wasiwasi, mali na anasa za maisha, na hawazai matunda yakakomaa.

15

Na zile zilizoanguka kwenye udongo mzuri ndio watu wale wanaolisikia lile neno, wakalizingatia kwa moyo mwema na wa utii. Hao huvumilia mpaka wakazaa matunda.

16

"Watu hawawashi taa na kuifunika kwa chombo au kuiweka mvunguni. Lakini huiweka juu ya kinara ili watu wanapoingia ndani wapate kuona mwanga.

17

"Chochote kilichofichwa kitafichuliwa na siri yoyote itagunduliwa na kujulikana hadharani.

18

"Kwa hiyo, jihadharini jinsi mnavyosikia; maana aliye na kitu ataongezewa, lakini yule asiye na kitu, hata kile anachodhani kuwa anacho, kitachukuliwa."

19

Hapo mama na ndugu zake Yesu wakamjia, lakini hawakuweza kumkaribia kwa sababu ya umati wa watu.

20

Yesu akapewa habari kwamba mama na ndugu zake walikuwa nje, wanataka kumwona.

21

Lakini Yesu akawaambia watu wote, "Mama yangu na ndugu zangu ni wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika."

22

Siku moja, Yesu alipanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, "Tuvuke ziwa twende mpaka ng`ambo." Basi, wakaanza safari.

23

Walipokuwa wanasafiri kwa mashua, Yesu alishikwa na usingizi, akalala. Dhoruba kali ikaanza kuvuma, maji yakaanza kuingia ndani ya mashua, wakawa katika hatari.

24

Wale wanafunzi wakamwendea Yesu, wakamwamsha wakisema, "Bwana, Bwana! Tunaangamia!" Yesu akaamka, akaikemea dhoruba na mawimbi, navyo vikatulia, kukawa shwari.

25

Kisha akawaambia, "Iko wapi imani yenu?" Lakini wao walishangaa na kuogopa huku wakiambiana, "Huyu ni nani basi, hata anaamuru dhoruba na mawimbi, navyo vinamtii?"

26

Wakaendelea na safari, wakafika pwani ya nchi ya Wagerase inayokabiliana na Galilaya, ng`ambo ya ziwa.

27

Alipokuwa anashuka pwani, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo alimjia kutoka mjini. Kwa muda mrefu mtu huyo, hakuwa anavaa nguo, wala hakuwa anaishi nyumbani bali makaburini.

28

Alipomwona Yesu, alipiga kelele na kujitupa chini mbele yake, na kusema kwa sauti kubwa "We, Yesu Mwana wa Mungu Aliye Juu una shauri gani nami? Ninakusihi usinitese!"

29

Alisema hivyo kwa kuwa Yesu alikwishamwambia huyo pepo mchafu amtoke mtu huyo. Pepo huyo mchafu alikuwa anamvamia mtu huyo mara nyingi, na ingawa watu walimweka ndani na kumfunga kwa minyororo na pingu, lakini kila mara alivivunja vifungo hivyo, akakimbizwa na pepo huyo mchafu hadi jangwani.

30

Basi, Yesu akamwuliza, "Jina lako nani?" Yeye akajibu, "Jina langu ni `Jeshi"`--kwa sababu pepo wengi walikuwa wamempagaa.

31

Hao pepo wakamsihi asiwaamuru wamtoke na kwenda kwenye shimo lisilo na mwisho. ic

32

Kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakilisha mlimani. Basi, hao pepo wakamsihi awaruhusu wawaingie. Naye Yesu akawapa ruhusa.

33

Kwa hiyo pepo hao wakamtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nao wakaporomoka kwenye ule mteremko mkali, wakatumbukia ziwani, wakazama majini.

34

Wale wachungaji walipoona yote yaliyotokea walikimbia, wakaenda kuwapa watu habari, mjini na mashambani.

35

Watu wakaja kuona yaliyotokea. Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mtu aliyetokwa na pepo ameketi karibu na Yesu, amevaa nguo, ana akili zake, wakaogopa.

36

Wale watu walioshuhudia tukio hilo waliwaeleza hao jinsi yule mtu alivyoponywa.

37

Wakazi wa nchi ya Gerase walishikwa na hofu kubwa. Kwa hiyo wakamwomba Yesu aondoke, aende zake. Hivyo Yesu alipanda tena mashua, akaondoka.

38

Yule mtu aliyetokwa na wale pepo akamsihi aende pamoja naye. Lakini Yesu hakumruhusu, bali akamwambia,

39

"Rudi nyumbani ukaeleze yote Mungu aliyokutendea." Basi, yule mtu akaenda akitangaza kila mahali katika mji ule mambo yote Yesu aliyomtendea.

40

Yesu aliporudi upande mwingine wa ziwa, kundi la watu lilimkaribisha, kwa maana wote walikuwa wanamngojea.

41

Hapo akaja mtu mmoja aitwaye Yairo, ofisa wa sunagogi. Alijitupa miguuni pa Yesu, akamwomba aende nyumbani kwake,

42

kwa kuwa binti yake wa pekee, mwana wa pekee mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa mahututi. Yesu alipokuwa akienda, watu wakawa wanamsonga kila upande.

43

Kulikuwa na mwanamke mmoja kati ya lile kundi la watu, ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote kwa waganga, hakuna aliyefaulu kumponya.

44

Huyo mwanamke alimfuata Yesu nyuma, akagusa pindo la vazi lake. Papo hapo akaponywa ugonjwa wake wa kutokwa damu.

45

Yesu akasema, "Ni nani aliyenigusa?" Wote wakasema kwamba hapakuwa na mtu aliyemgusa. Naye Petro akasema, "Mwalimu, umati wa watu umekuzunguka na kukusonga!"

46

Lakini Yesu akasema, "Kuna mtu aliyenigusa, maana nimehisi nguvu imenitoka."

47

Yule mwanamke alipoona kwamba hawezi kujificha, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa mbele ya Yesu. Hapo akaeleza mbele ya wote kisa cha kumgusa Yesu na jinsi alivyoponyeshwa mara moja.

48

Yesu akamwambia, "Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani."

49

Alipokuwa bado akiongea, Yairo akaletewa habari kutoka nyumbani: "Binti yako ameshakufa, ya nini kumsumbua Mwalimu zaidi?"

50

Yesu aliposikia hayo akamwambia Yairo, "Usiogope; amini tu, naye atapona."

51

Alipofika nyumbani hakumruhusu mtu kuingia ndani pamoja naye, isipokuwa Petro, Yohane, Yakobo na wazazi wa huyo msichana.

52

Watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili yake. Lakini Yesu akawaambia, "Msilie, kwa maana mtoto hajafa, amelala tu!"

53

Nao wakamcheka kwa sababu walijua kwamba alikuwa amekufa.

54

Lakini Yesu akamshika mkono akasema, "Mtoto amka!"

55

Roho yake ikamrudia, akaamka mara. Yesu akaamuru wampe chakula.

56

Wazazi wake walishangaa, lakini Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote hayo yaliyotendeka.

Luke 9

 

 

 

Public Domain Software by johnhurt.com