Swahili New Testament Bible

Revelation 8

Revelation

Return to Index

Chapter 9

1

Kisha malaika wa tano akapiga tarumbeta yake. Nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka juu ya nchi kutoka mbinguni. Nayo ikapewa ufunguo wa shimo la Kuzimu.

2

Basi, nyota hiyo ikafungua shimo la Kuzimu, kukatoka moshi wa tanuru kubwa. Jua na anga vikatiwa giza kwa moshi huo wa Kuzimu.

3

Nzige wakatoka katika moshi huo, wakaingia duniani wakapewa nguvu kama ya ng`e.

4

Wakaamrishwa wasiharibu nyasi za nchi wala majani wala miti yoyote, bali wawaharibu wale tu ambao hawakupigwa mhuri wa Mungu katika paji la uso.

5

Nzige hao hawakuruhusiwa kuwaua watu, ila kuwatesa tu kwa muda wa miezi mitano. Maumivu watakayosababisha ni kama maumivu yanayompata mtu wakati anapoumwa na ng`e.

6

Muda huo watu watatafuta kifo lakini hawatakipata; watatamani kufa lakini kifo kitawakimbia.

7

Kwa kuonekana, nzige hao walikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita. Juu ya vichwa vyao walikuwa na taji zilizo kama za dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu.

8

Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake, na meno yao yalikuwa kama meno ya simba.

9

Vifua vyao vilikuwa vimefunikwa kitu kama ngao ya chuma. Sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya msafara wa magari ya farasi wengi wanaokimbilia vitani.

10

Walikuwa na mikia na miiba kama ng`e, na kwa mikia hiyo, walikuwa na nguvu ya kuwadhuru watu kwa muda wa miezi mitano.

11

Tena wanaye mfalme anayewatawala, naye ndiye malaika wa kuzimu; jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kigiriki ni Apolioni, yaani mwangamizi.

12

Maafa ya kwanza yamepita; bado mengine mawili yanafuata.

13

Kisha malaika wa sita akapiga tarumbeta yake. Nami nikasikia sauti moja kutoka katika pembe nne za madhabahu ya dhahabu iliyokuwa mbele ya Mungu.

14

Sauti hiyo ikamwambia huyo malaika wa sita mwenye tarumbeta, "Wafungulie malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa `Eufrate!"`

15

Naye akawafungulia malaika hao wanne ambao walikuwa wametayarishwa kwa ajili ya saa hiyo ya siku ya mwezi huo, wa mwaka huohuo, kuua theluthi moja ya wanaadamu.

16

Nilisikia idadi ya majeshi wapanda farasi ilikuwa milioni mia mbili.

17

Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapanda farasi katika hiyo njozi: Walikuwa na ngao vifuani zilizokuwa moto mtupu, zenye rangi ya samawati na njano kama kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vya simba; na moto, moshi, na kiberiti vilikuwa vinatoka kinywani mwao.

18

Theluthi moja ya wanaadamu waliuawa kwa mabaa hayo matatu yaani, moto, moshi na kiberiti, yaliyokuwa yanatoka katika vinywa vyao;

19

maana nguvu ya farasi hao ilikuwa vinywani mwao na katika mikia yao. Mikia yao ilikuwa na vichwa kama nyoka, na waliitumia hiyo kuwadhuru watu.

20

Wanaadamu wengine waliobaki ambao hawakuuawa na mabaa hayo, hawakugeuka na kuviacha vitu walivyokuwa wametengeneza kwa mikono yao wenyewe; bali wakaendelea kuabudu pepo, sanamu za dhahabu, fedha, shaba, mawe na miti, vitu ambavyo haviwezi kuona, kusikia wala kutembea.

21

Wala hawakutubu na kuacha kufanya mauaji, uchawi, uzinzi, na wizi.

Revelation 10

 

 

 

Public Domain Software by johnhurt.com